Mbunge
wa Jimbo la Kigoma Kusini David Kafulila amewajibu baadhi ya wakazi wa jimbo hilo waliokuwa
wakidai mbunge huyo atahamia chama cha ACT kwa kuchukua fomu ya kuwania tena
nafasi hiyo kupitia chama cha NCCR
Mageuzi.
Akizungumza
baada ya kuchukua fomu ya ubunge hapo jana, Kafulila alisema kuwa yeye bado ni
mwanachama wa NCCR Mageuzi na ataendelea kuwatumia wananchi kupitia chama hicho
ambacho kwake anakiona ndio bora.
Kafulila akiwapungia mkono wakazi wa Nguruka waliofurika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Nguruka kushuhudia tukio la kuchukua fomu kuwania tena nafasi hiyo. |
“Nadhani
kitendo nilichofanya leo cha kuchukua fomu kitawafanya msiendelee kuamini
minong’ono ya watu pia kwa kauli yangu mwenyewe nasema siwezi kuhamia chama cha
ACT-Wazalendo” alisisitiza.
Aidha
Kafulila ambaye aliwasili jimboni kwake Jana na kupata mapokezi makubwa kutoka
Kwa wakazi wa Nguruka na baadaye kukabidhiwa fomu ya ubunge na wazee wa kata ya
Nguruka wakiongozwa na Sheikh Rajabu Kagina, baada ya kulipia kiasi cha
shilingi elfu 50.
Kafulila akionyesha fomu ya kugombea ubunge jimbo la Kigoma Kusini kupitia NCCR Mageuzi, baada ya kukabidhiwa na wazee wa Kata ya Nguruka wakiongozwa na Sheikh Rajabu Kazina. |
Baada
ya kukabidhiwa fomu hiyo Kafulila aliwashukuru wananchi wa Jimbo la Kigoma
Kusini kwa ushirikiano waliompa katika kuleta maendeleo na kisha kuelezea
mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano yeye akiwa Mbunge.
Alisema
kuwa katika kipindi chake kinachomalizika amejitahidi kwa asilimia kubwa kuleta
mabadiliko jimboni ambapo ameweza kutatua baadhi ya kero za wananchi ikiwemo
kusomesha watoto 200 ambao wazazi wao hawana uwezo wa kugharamia masomo.
Alieleza
mafanikio mengine kuwa ni pamoja na kununua vifaa vya maabara kwa shule za kata
17 zilizoko jimboni humo, vitanda na magodoro kwa ajili kina mama kujifungulia
katika kituo cha afya Nguruka na kumaliza tatizo la kina mama kulala wawili
wawili kwenye kitanda kimoja.
Aidha
alieleza kuwa amesaidia kuchimba visima vya maji katika baadhi ya vijiji
ikiwemo Kijiji cha Mtego wa Noti na kijiji cha Muganza pamoja na kuwezesha
wakazi wa vijiji hivyo na vijiji Jirani kupata mawasiliano ya simu na barabara.
Nao
baadhi ya wakazi wa Kata ya Nguruka wakiwemo Bernard Banama, Mathayo James na
Mariam Sigele, walipoulizwa walisema yote yaliyoelezwa na Mbunge wao ni sahihi
kuwa ameleta tofauti ukilinganisha na wabunge waliotangulia na kwamba wao
wataendelea kumuunga mkono na kuahidi kumchagua tena mwezi Octoba.
Mwisho.