Kigoma Online News

FURNITURE

KALIHAMWE STATIONARY

KALIHAMWE STATIONARY

Jul 29, 2015

WAGOMBEA CCM KIGOMA WALALAMIKIA MCHEZO MCHAFU NDANI YA CHAMA HICHO


WAKATI vyama vya siasa vikiendelea kuandaa wagombea ambao watapigiwa kura za maoni ili kupata wagombea wa viti vya ubunge mkoani Kigoma, hali si shwari kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Uvinza (Kigoma Kaskazini) baada ya wagombea kulalamikia mchezo mchafu unaofanywa na viongozi wa juu katika wilaya hiyo kwa kutaka kuwabeba baadhi ya wagombea katika kura za maoni.


Wakizungumza na waandishi wa habari mapema wiki hii baadhi ya wagombea hao walisema kuwa, katika maeneo mengi waliyopita wamebaini kuwa viongozi wa matawi wamepeleka wilayani taarifa za idadi ya wanachama ambazo sio sahihi na zina lengo la kuwabeba wanachama Fulani, jambo ambalo ni hatari na linaweza kukigawa chama.

Miongoni mwa wagombea hao ni Mwanasheria  Idd Ndabhona, ambaye alisema kuwa taarifa za idadi ya wanachama kwenye matawi zinazopelekwa wilayani sio sahihi na zinakinzana kwa kiasi kikubwa na taarifa za wanachama zilizoko kwenye rekodi  ya matawi husika.

Ndabona alisema kuwa,  tawi la Kandaga ambalo taarifa za wanachama zilizopelekwa wilayani ni 1,086 lakini taarifa zilizoko kwenye tawi hilo zinaonyesha kuwa wanachama waliosajiliwa ni 800, jambo ambalo limejitokeza pia katika tawi la Mlela.

“Wote tumeshuhudia na tumewakabidhi viongozi wa chama wilaya, lakini kwa kweli inaonekana wazi kwamba viongozi katika ngazi za matawi wamepeleka taarifa ambazo si sawa kwa lengo la kuwabeba wagombea fulani na pengine kutengeneza kura za maruhani lakini tunaamini kwamba chama kitalishughulikia suala hilo,”alisema Ndabhona.

Aidha Hasna Mwilima ambaye pia ni mgombea, alihoji kuhusu kata ya Igalula ambayo kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, ina wakazi elfu 11 lakini kwa takwimu walizopewa na katibu wa CCM wilaya ya Uvinza, wanachama wa CCM ni  9,777, jambo ambalo alisema haliingii akilini.

“Ina maana basi hata watoto wadogo wenye umri wa chini ya miaka 18 ni wanachama wa CCM! Sasa inatupa mashaka; na inatupa mashaka pale ambapo tunapata takwimu za mtendaji mkuu ndani ya wilaya, halafu watendaji wa chini ambao ndio wenye wanachama na ndio wanaojua wana takwimu tofauti” alisema Mwilima.

Nae kiongozi wa wagombea hao, Manju Msambya, alisema katika kampeni za wagombea kujinadi kwa Wanachama wa CCM walibaini dosari mbali mbali ikiwemo kadi bandia pamoja na takwimu za idadi ya wanachama kwenye matawi kupishana na zile zilizotolewa na Katibu wa CCM Wilaya ya Uvinza, Mohamed Gwama.

“Kwa mfano tumepata kadi zenye namba A.I. 8149645, A.I. 8149639 na Kadi namba A.I. 8149250 sio kadi zinazopaswa kutumika wilaya ya Uvinza na mkoa wa Kigoma, na hii inamaanisha kuna mtu ameziingiza kutoka mkoa mwingine kwa maslahi yake binafsi au ya mtu fulani,” alisema Msambya.

Akizungumzia malalamiko hayo Kiongozi Mkuu wa Msafara wa Wagombea, Gervas Kengwa, ambaye ni mjumbe wa kamati ya siasa ya CCM Wilaya ya Uvinza, amekiri kuwepo kwa wanachama hewa wanaondaliwa kwa lengo la kumbeba mmoja wa wagombea.

“Kuna dalili za uchakachuaji, kwa hiyo tumemweleza katibu wa wilaya afuatilie jambo hili ili kabla ya wakati wa kupiga kura tatizo hilo liwe limemalizika,”alisema Kengwa.

Kufuatia sintofahamu hiyo wagombea hao wameandika barua kwenda kwa Katibu wa CCM Wilaya ya Uvinza na nakala kwa Katibu Mkuu wa CCM Taifa na Katibu wa CCM Mkoa wa Kigoma wakilalamikia kuwepo wanachama hewa na takwimu zisizo sahihi zinazodaiwa kutolewa na Katibu wa CCM katika Wilaya hiyo.

Alipoulizwa juu madai hayo katibu wa CCM Wilaya ya Uvinza, Mohamed Gwama, amekana kuhusika na hujuma dhidi ya wagombea, ambapo alisema kuwa wameanza kushughulikia malalamiko hayo kwa kutembelea matawi yote ili kuhakiki idadi ya wanachama waliopo.

Nae Katibu wa CCM Mkoa wa Kigoma, Naomi Kapambala, alisema kadi zote ziligawanywa kwa utaratibu maalumu kwa ajili ya kuepuka baadhi ya Wagombea kununua kadi kiholela na kuwagawia Wanachama wanaoamini watawachagua wakati wa kupiga kura za maoni.

Aliongeza kuwa ili kuondoa tatizo hilo majina yote ya wapiga kura ambao ni wanachama hai wa CCM yatabandikwa kwenye mbao za matangazo katika ofisi za matawi na Kata zote kabla ya zoezi la upigaji kura kuanza ili kila mmoja aone kama anastahili kupiga kura au la.

Hata hivyo wagombea hao walisema katika barua yao kuwa enadapo chama kitashindwa kuchukua hatua kutatua tatizo hilo kuna uwezekano mkubwa Jimbo hilo likaendelea kutawaliwa na Chama cha NCCR Mageuzi.

Jumla ya wagombea wanaoomba ridhaa ya kuteuliwa na chama cha mapinduzi ili kupeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao ni 13.

Katika uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2010 David Kafulila wa NCCR Mageuzi, alimbwaga aliyekuwa mgombea wa CCM, Kifu Gulam Hussein Shabani, baada ya wagombea wa CCM kuhujumiana kwenye kura za maoni.