Mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali ya mkoa Kigoma zimeleta athari kwa kuharibu
miundomibinu ya madaraja katika mfereji wa Lubengera uliopo Manispaa ya Kigoma Ujiji unaotumika
kupitisha maji machafu kwenda ziwa Tanganyika.
Kufuatia kubomoka kwa madaraja hayo
na serikali kulazimika kuifunga barabara ya Kaya Road ambayo daraja la kwa
Jaffar limaethiriwa na mvua hiyo wananchi wamelalamikia viwango duni vya ujenzi
wa madaraja hayo uliofanywa na makandarasi wazawa na hivyo kuitia hasara
serikali.
Wakizungumza kuhusiana na hali hiyo
Mussa Abbasi na Ayubu Mlagile wamesema kuwa badala ya serikali kuendelea
kupoteza mamilioni ya shilingi kuwapa wakandarasi wazawa miradi hiyo ya ujenzi
wa madaraja na kuharibika baada ya vipindi vifupi wametaka kazi hiyo wapewe
wakandarasi wa makampuni ya kichina kutokana na utaalam walionao na vifaa vya
kisasa vya kufanyia kazi.
Akizungumzia kubomoka kwa madaraja
hayo Diwani wa kata ya Kigoma Mjini,Hussein Kalyango amesema kuwa tayari
viongozi mbalimbali wa serikali akiwemo Mkuu wa mkoa Kigoma, Issa Machinya
wametembelea kuona uharibifu huo na kwamba Hamashauri itachukua hatua za haraka
kukabiliana na uharibifu huo.