Kigoma Online News

FURNITURE

KALIHAMWE STATIONARY

KALIHAMWE STATIONARY

Jan 18, 2016

WAKIMBIZI 1808 WAKAMATWA KIGOMA

Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma, Naibu Kamishina  Maurice Kitinusa, akizungumzia zoezi la kukamata wahamiaji waishio nchini bila vibari.
Idara ya Uhamiaji mkoani Kigoma imefanikiwa kukamata wahamiaji 1808 wanaoishi nchini bila vibali mara baada ya kuanza zoezi hilo katika Wilaya zote mkoani humo mwanzoni mwa mwaka jana.

Akizungumza na blog hii hapo jana, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma Naibu Kamishina  Maurice Kitinusa, alisema kuwa,  takwimu hiyo ni kuanzia mwezi Aprili mwaka jana mpaka mwezi Januari mwaka huu.

Alisema kuwa, baada ya kuwakamata  wahamiaji hao wapo waliorudishwa nchini kwao na wengine kupelekwa mahakamni huku wengine wakipunguziwa vibari vyao vya kuishi nchini baada ya kukiuka sheria.

Aidha Kitinusa alisema kuwa, wahamiaji 453 walipelekwa mahakamani ili kuchukuliwa hatua za kisheria ambapo katika hao 15 walihararisha ukazi wao baada ya kupewa vibari vya muda mfupi (CTA) na wahamiaji 750 walifukuzwa nchini baada ya kukutwa na makosa.

“Katika idadi hiyo watu 117 tuliwakabidhi kwa idara ya wakimbizi baada ya kugundua kuwa ni wakimbizi waliokuwa wakiishi vijijini, pia watu 206 tuliwaachia huru baada ya kuthibitisha uharari wao wa kuwepo nchini baada ya kuleta vitambulisho ambavyo wakati wanakamatwa hawakuwa navyo” alisema Kitinusa.

Kitinusa aliongeza kuwa, kuna watu 104 ambao walifupishiwa vibali vyao vya kuwepo nchini baada ya kuonekana  hawana sababu za msingi zilizowaleta nchini kama walikuwa na vibali vya miezi mitatu walipunguziwa mpaka wiki moja wawe wameondoka.

 “Pia kuna watuhumiwa 163 ambao uraia wao unautata mana wao  wanasema ni raia  watanzania lakini viashiria vingi vinaonyesha sio raia wa watanzania kwahiyo hawa uchunguzi unaendelea kulingana na taarifa walizozitoa” alisema Kitinusa.

Pamoja na hayo Kitinusa aliwataka watanzania ambao wanamiriki nyumba za kulala wageni kufuata sheria inayowataka kuwaorodhesha wageni wote wanaofika katika nyumba zao ili kufahamu kama wamepata wageni ambao sio raia.

“Mpaka sasa kuna tuna keshi tatu mahakamani za wamiriki wa nyumba za wageni kwa makosa ya kuwalaza wahamiaji wasio na vibari, na ifahamike kuwa kuwalaza watu bila kuwaorodhesha ni makosa awe mtanzania au raia kutoka nchi nyingeine na sisi tunawapeleka mahakamani wanaokutwa na makosa hayo pia wale ambao wanawapokea wageni na kukaa nao bila kutoa taarifa katika ofisi za uhamiaji sambamba na wanaowatumikisha mashambani” alisema Kitinusa.

Hata hivyo Kitinusa alisema kuwa,  zoezi la kukamata wahamiaji waishio nchini bila vibali ni endelevu na Idara ya Uhamiaji mkoani Kigoma inafanya zoezi hilo kila siku katika Wilaya zote za mkoa huu.