Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma John Ndungulu akizungumza na waandishi wa habari hii leo kuhusu kusimamishwa kazi kwa watumishi 9 wa Manispaa ya Kigoma-Ujiji. |
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma John Ndungulu wa kwanza kulia, akizungumza na waandishi wa habari hii leo kuhusu kusimamishwa kazi kwa watumishi waManispaa ya Kigoma-Ujiji. |
Watumishi
tisa wa Manispaa ya Kigoma-Ujiji
wamesimamishwa kazi mara baada ya kubainika kuingia mikataba mibovu isiyokuwa
na tija na kuisababishia Manispaa hasara ya kupoteza mapato sambamba na kulipa
fidia ambazo ni batiri pamoja na kuuza mali za Halmashauri kinyume cha sheria.
Maamuzi
hayo yamefikiwa na ofisi ya Mkoa wa Kigoma baada ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, kubaini uuzwaji huo na kumuagiza Katibu
Tawala wa Mkoa huu, kufanya uchunguzi wa awali kuhusu tuhuma hizo ambapo alitakiwa kutoa mrejesho
Januari 2 katika ofisi ya Waziri Mkuu.
Akizungumza
na waandishi wa habari hii leo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, John Ndungulu,
amesema, baada ya kuagizwa na Waziri Mkuu, aliunda kamati ya uchunguzi wa awali
ambapo kabla ya Januari 2 walikuwa wameshakamilisha uchunguzi wa tuhuma hizo.
Alisema
kuwa, awali tuhuma ambazo alizibaini Waziri Mkuu ni pamoja na uuzwaji wa
majengo ya Manispaa likiwemo Jengo la Maendeleo ya Mkoa (KIGODEKO) lenye kiwanja
namba 551 na Miboss lenye kiwanya namba 295 ambapo watuhumiwa walidai kuwa
waliuza viwanja badala ya majengo.
“Tuhuma
zingine zinazowakabiri watumishi hao ni manunuzi hewa ya vipuri vya gari SM 553
gari aina ya tipa vyenye gharama ya TSH. 8,002,000, Ununuzi hewa wa sajala
yenye thamani ya Tshs. 4,640,000, matumizi mabovu ya fedha za serikali kwaajiri
ya matengenezo ya barabara yenye thamani ya Tsh. 18,000,000 kwa ajiri ya
matengenezo na Tsh. 48,000,000 kwaajiri ya mkataba ambao haukufanyiwa kazi na
matumizi yasiyoidhinishwa ya Tshs 809,633,407 ambazo zilitengwa kwaajiri ya
miradi ya maendeleo badala yake zikapelekwa kwenye ujenzi wa maabara” amesema
Ndungulu.
Aidha
Ndungulu amesema, uchunguzi wa awali uliofanywa na kamati ulibaini kuwa watendaji wa Manispaa
waliingia mikataba mibovu isiyokuwa na tija na kuisababishia Manispaa hasara ya
kupoteza mapato sambamba na kulipa fidia ambazo ni batiri, baadhi ya watendaji
kushiriki katika ubadirifu wa uuzwaji wa mali za Manispaa bila kufuata
utaratibu, ukodishaji wa jengo la KIGODEKO bila kufuata sheria.
Ndungulu
amesema, baada ya kubainika kwa tuhuma hizo ofisi ya mkoa imeamua kuwasimamisha
kazi watumishi hao ili kupisha uchunguzi zaidi kuhusu tuhuma hizo ambapo
uchunguzi zaidi ukikamilika hatua zingine za kisheria zitafanyika.
Aliwataja
majina watumishi waliosimamishwa kazi kuwa ni Wilfred Mwita (Mkuu wa Idara
ya Mipango Manispaa), Emmanuel Mkwe (Mwanaseheria wa
Manispaa), Mhandisi Boniface William (Mhandisi wa Manispaa), Mussa Igugu (Mkuu
wa Kitengo cha Biashara), Elimboto Zacharia (Mkaguzi wa Ndani wa Manispaa),
Leonard Nzirailunde (Afisa Misitu), Shida Thadei (Afisa Ugavi), Gwawili Mkoka
(Mhasibu wa Manispaa) na Omary Hassan (Fundi Mkuu wa Magari).
Hata
hivyo Ndungulu amesema, Ofisi ya Mkoa imemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri
Mhandisi Boniface Nyambele, kusimamia urejeshwaji wa mali za Manispaa
zilizouzwa bila kufuata sheria na taratibu.
“Pia
tumewaagiza jeshi la polisi na TAKUKURU kuchunguza tuhuma hizo kama kuna mianya
ya rushwa ili kama kuwa watu walihusika katika utioaji wa rushwa basi nao
washughurkiwe kwa mujibu wa sheria” amesema Ndungulu.