Kigoma Online News

FURNITURE

KALIHAMWE STATIONARY

KALIHAMWE STATIONARY

Feb 9, 2016

WANAFUNZI SHULE YA MSINGI AIRPORT HATARINI KUPATA MAGONYWA YA MLIPUKO


Picha sio za shule husika
Zaidi ya wanafunzi 1490 wa shule ya msingi Airport katika Manispaa ya Kigoma-Ujiji wako hatarini kupata magonjwa ya mlipuko kutokana  na vyoo wanavyotumia kukosa maji hivyo kupelekea uchafu kuzagaa hovyo.

Wakizungumza na Jembe FM hii leo, baadhi ya walimu shuleni hapo ambao wameomba majina yao kutokutajwa,  kwa nyakati tofauti wamesema, kero ya vyoo shuleni hapo  ni ya muda mrefu na uongozi wa sekta ya elimu unafahamu lakini hakuna utekelezaji unaofanyika.

Wamesema licha ya vyoo hivyo kukosa maji ambapo wanafunzi hujisaidia haja kubwa na ndogo bila kutumia maji jambo linalosababisha  uchafu kuzagaa pia vyoo hivyo viko hatarini kubomoka kutokana na kutofanyiwa ukarabati baada ya mvua kuendelea kunyesha mkoani hapa.

Aidha Wameongeza kuwa, shule hiyo ina zaidi ya wanafunzi 1490 huku ikiwa na matundu ya vyoo 11 lakini yanayotumika ni matundu matatu tu wakati yaliyosalia yakiwa yamejaa uchafu wa vinyesi na wadudu.

Wamesema, kama maji yangepatikana shuleni hapo wangejitahidi kufanya usafi katika vyoo hivyo ili matundu yote yatumike lakini kutokana na kukosekana kwa maji hari ya usafi shuleni hapo imekuwa ngumu kutekelezeka.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kigoma ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Saveli Mwangasame, amekiri kuwepo kwa tatizo hilo na kusema kuwa si shule hiyo pekee bali shule nyingi za msingi wilayani hapa zinakabiliwa na matatizo ya ukosefu wa matundu ya vyoo, madawati na madarasa.