Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, SACP Frednand Mtui |
Akizungumzia tukio hilo Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Kigoma, SACP Fredinand Mtui amesema kuwa tukio hilo lilitokea June, 30 katika Wilaya ya Kasulu baada ya watu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kuvamia duka la Emanuel Frednand wakitaka awape mauzo ya siku hiyo.
Kamanda amesema wakati majambazi hao wakiendelea kumtaka Bwana Frednand kuwapatia pesa za mauzo ndiyo marehemu ambae alikuwa ni mlinzi wa duka hilo alipoingilia ugomvi huo akipinga kitendo cha boss wake kuwapa majambazi pesa hizo.
Kamanda amesema kuwa baada ya kuingilia ugomvi huo ndipo majambazi hao walipompiga marehemu risasi maeneo ya shingoni na kupelekea kifo chake.
Kamanda Mtui |
Aidha Kamanda majambazi hayo yalimchoma na kisu mmiliki wa duka katika eneo la bega na kukimbia kusipojulikana baada ya kugundua kuwa tayari askari wa doria walikuwa wakiwafatilia.
Ameongeza kuwa baada ya askari kufika eneo la tukio walikuta bunduki aina ya SMG yenye namba za usajili M70AB 2-691108 ikiwa na risasi29 na kuokotwa ganda la risasi moja katika eneo hilo.
Amesema kuwa majeruhi alipelekwa hospitali ya Wilaya ya Kasulu kupata matibabu na baadae aliruhusiwa kutoka.
Aidha Kamanda ametoa wito kwa wananchi wa mkoa wa Kigoma kuwataka waendelee kushirikiana na Jeshi la Polisi ili kupunguza vitendo vya uharifu.