MKOA wa Kigoma umekumbwa na adha ya
upungufu mkubwa wa vifaa tiba katika vituo vyake vya afya, zahanati na
hospitali, hali inayotishia usalama wa wananchi.
Aidha hiyo inatokana na kuwepo kwa
wimbi kubwa la raia kutoka nchini Burundi wanaoingia mkoani hapa kutafuta
hifadhi, kufuatia machafuko ya kisiasa yanayoendelea katika nchi hiyo jirani.
Hayo yalielezwa na Mganga Mkuu wa
Mkoa wa Kigoma, Dk. Leonard Subi alipokuwa akipokea msaada wa vifaa tiba,
vilivyotolewa na Shirika la Actionaid, katika hafla iliyofanyika juzi.
Baadhi ya vifaa tiba na magodoro yakishushwa katika hospitali ya mkoa mwa Kigoma Maweni baada ya kukabidhiwa. |
Alisema kuwa hivi sasa vituo vingi
vya kutoa huduma za afya mkoani Kigoma vinakabiliwa na tatizo hilo la upungufu
wa vifaa tiba, huku kukiwa na changamoto nyingine ya magonjwa ya kuhara na
kipindupindu ambapo watu 38 walisharipotiwa kufariki dunia.
“Baada ya magonjwa ya mlipuko
kutokea kutokana na hari ya uchafu iliyosabishwa na kutokuwepo kwa huduma za
kijamii zenye kukidhi wingi wa watu, Serikali ya mkoa kwa kushirikiana na
idara ya afya mkoani hapa tulijitahidi kutoa huduma kwa wagonjwa ambao
wengi wao walikuwa wakimbizi.
“Kufuatia hali hiyo, vifaa tiba
vilivyokuwa vikitumika ni vile vilivyowekwa kwa ajiri ya Watanzania kabla ya
mashirika mengine kuanza kutoa msaada wa vifaa hivyo,” alisema Mganga Mkuu huyo
wa Mkoa wa Kigoma.
Mkuu wa mkoa wa Kigoma Issa Machibya katikati akipokea baadhi ya vifaa tiba kutoka kwa Dk. Azaveli Lwaitama ambaye ni Muhadhiri Mwandamizi na Mwenyekiti Msaidizi wa wa Shirika la Actionaid Tanzania. |
Dk. Subi alisema hadi sasa kuna
wakimbizi wapao 100,025 walioko kambi ya Nyarugusu, ambapo Vijiji vya
Mwakizega, Ilagara, Kalago Wilaya ya Uvinza, Kaseke na Manispaa ya Kigoma kuna
wagonjwa wa kipindupindu walioripotiwa kufikia idadi ya watu wanane.
Kwa upande wake Mkuu wa Programu na
Sera wa Shirika la Action Aid, Josephat Mshigati alisema kwenye hafla hiyo
kuwa, shirika hilo limetoa dawa, vitendanishi, magodoro, groves (medicines and
medical supplies/ equipment) kwa Serikali ya mkoa wa Kigoma.
Baadhi ya vifaa tiba na magodoro yakishushwa katika hospitali ya mkoa wa Kigoma Maweni baada ya kukabidhiwa. |
“Vifaa hivi vimegharimu kiasi cha
sh. 65,425,000 ambapo ukijumlisha na usafiri wake inakuwa sh. 73,425,000.
Lakini pia tumefanya hivi ili kuyakumbusha mashirika mengine kuungana na sisi
kutoa msaada wa vifaa tiba ili kumaliza kabisa tatizo hili,” alisema Mshigati.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Dk. Leonard Subi akizungumza wakati wa kukabidhiwa vifaa tiba. |