WAZEE
wa Kijiji cha Kiganza Kata ya Mwandiga katika Jimbo la Kigoma Kaskazini
lililoko Wilaya ya Kigoma Vijiji wamemchukulia fomu ya kugombea Ubunge wa Jimbo
hilo Mjumbe wa Kuchaguliwa Kamati Kuu Taifa CHADEMA, Dkt. Yared Fubusa kupitia
Chama hicho baada ya kuona anafaa kuongoza jimbo lao kutokana na kukerwa na
tabia za Wabunge waliopita.
Akizungumza
kwaniaba ya Wazee wenzake hapo jana wakati wakimkabidhi fomu hiyo, Mwenyekiti
wa Wazee Wilaya ya Kigoma (CHADEMA) Mzee Yasini Athumani (Mapigosaba) alisema
kuwa, Kiu yao kubwa ni kupata mbunge ambaye atakaa na wananchi na kufahamu
matatizo yao badala ya kwenda kuishi Dar es Salaam baada ya kuchaguliwa.
Mwenyekiti wa Wazee Wilaya ya Kigoma, Mzee Yasini Athumani (Mapigosaba) akimkabidhi fomu Dkt. Yaredi Fubusa |
Alisema
kuwa, baada ya Zitto Kabwe kushindwa kulitumikia Jimbo lake sambamba na kufukuzwa
katika chama walikaa wao kama wazee wa Kijiji cha Kiganza na kutafuta ni nani
anayeweza kuwa Mbunge wao ambaye ataweka mbele maslahi ya Jimbo.
“Tuliona
Dkt Yared anatufaa sana kulingana na tabia aliyoionyesha kwa wananchi wa
Kiganza sambamba na mchango mkubwa wa Elimu anaoutoa katika Jimbo vitu ambavyo
havikufanywa na Wabunge waliopita” Alisema Athumani.
Mjumbe wa Kuchaguliwa Kamati Kuu Taifa CHADEMA, Dkt Yaredi Fubusa akizungumza na wananchi baada ya kukabidhiwa fomu na wazee wa Jimbo la Kigoma Kaskazini |
Mzee
Athumani alisema, Licha ya kuwa Fubusa ni Mjumbe wa Kamati Kuu CHADEMA Taifa hilo wao hawakuangalia walichoangalia
ni elimu aliyonayo na mali alizo nazo lakini hakupenda kuishi kwenye mikoa
iliyoendelea bali anaishi na wanakijiji wenzake huku akitumia Elimu yake na
mali zake kuwasaidia wananchi.
“Moyo
wake wa Upendo kwa watu wa kijiji chake unatufanya tuamini ndie anayeweza
kutuwakilisha kwani kama amejenga shule mbalimbali katika jimbo hili akiwa ni
mwananchi wa kawaida basi anaweza kufanya makubwa akiwa Mbunge” aliongeza Mzee
Athumani.
Kwa
mujibu wa Mzee Athumani, walichukua Fomu hiyo kwa gharama ya shilingi 27000/=
na kuamini kuwa kumchukulia fomu itakuwa faida kwao kwani watakuwa na uwezo wa
kumbana endapo itatokea akikosea.
“Tunamuomba
Yaredi atutoe aibu Jimbo la Kigoma Kaskazini kuwa nyuma kimaendeleo na asiwe
kama wale Wabunge waliopita ambao wakifika Bungeni kazi yao ni kuongelea BUZWAGI,
EPA na ESCROW na kusahau kulizungumzia jimbo lao” alisisitiza Mzee Athumani.
Kwa
upande wake Mjumbe wa Kuchaguliwa Kamati
Kuu CHADEMA Taifa, Dkt Yaredi Fubusa, aliwashukuru wazee hao kwa kuona umuhimu
wake kwa jamii na kumuamini na kumpa dhamana ya kuwatumikia kama Mbunge.
Fubusa
alisema, kitendo cha wazee kumchukulia Fomu kimempa hamasa ya kuanza kufikilia
ni wapi ataanzia katika kuwatetea wananchi baada ya kuchaguliwa na kuwaahidi
kutokuwaangusha kama atapitishwa na CHADEMA kugombea Ubunge wa Jimbo hilo.
“Ni
bora ningechukua fomu mwenyewe kidogo ningejitetea pindi nikikosea lakini kama wamenichukulia wao basi hapo
sitakuwa na cha kujitetea ila nachowaahidi nipo kwaajiri ya kuwatumikia kama
walivyoniamini” alisema Fubusa.
Wakati
huohuo, waliotangza nia ya kugombea nafasi ya Ubunge katika majimbo mbalimbali
mkoani Kigoma wameendelea kurejesha fomu hizo na kusubiri iwapo watapewa nafasi
na CHADEMA ya kugombea nafasi ya ubunge katika Uchaguzi ujao.
Basilius
Budida ambaye alichukua fomu ya kuwania nafasi ya kugombea Ubunge katika Jimbo
la Manyovu alirejesha fomu hiyo hapo jana na kuwataka wananchi kumuunga mkono
endapo atapitishwa na chama chake.
“Uchaguzi
wa mwaka 2010 sikupata ushindi baada ya kufanyika kwa ufedhuri katika kura
zilizopigwa na kutoa nafasi kwa mgombea wa CCM ila mwaka huu nawaomba wananchi
kujitokeza kwa wingi ili kuwaonyesha walioiba kula mwaka jana kuwa mwaka huu ni
wa Upinzaji kuchukua madaraka” alisema Budida.