MFUKO
wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umekabidhi vitambulisho vya uanachama wa mfuko
huo kwa Waandishi wa Habari Mkoa wa Kigoma waliojiunga na mfuko huo ambao
huwanufaisha wanachama wake kupata huduma za matibabu bure katika hospitali na
zahanati ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Akikabidhi
vitambulisho hivyo hapo jana katika Ofisi za Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa
wa Kigoma (KGPC), Meneja wa NHIF, mkoani hapa, Elias Odhiambo, sambamba na
kuwapongeza wanahabari hao kwa hatua waliochukua pia aliwataka kuwa mabarozi
wazuri kwa vyama vingine vya wanahabari.
Alisema
kuwa, KGPC inaonyesha mfano kwa vyama vingine ambavyo bado havijajiunga pia ukomavu
katika kujari afya zao na matumizi ya pesa, na ni moja ya Vyama vichache ambavyo wanachama wake wamejiunga na
mfuko huo, hivyo KGPC inakuwa mfano kwa vyama ambavyo bado havijajiunga.
“Hapa
nchi kuna vyama vingi vya wanahabari katika kila mkoa ila ni vyama vichache
ambavyo vimejiunga na NHIF, hivyo tumaini letu ni kwamba mtawahamasisha hata
wengine kujiunga katika mfuko huu” alisema Odhiambo.
Aidha
Odhiambo aliongeza kuwa, NHIF ina manufaa makubwa kwa mtu anaejiunga na mfuko
kwani huchangia mara moja tu na baada ya kuchangia atatibiwa bure popote pale nchini katika kipindi cha mwaka mzima.
Hata
hivyo aliwataka wanahabari kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu faida za
mfuko huo ambazo kimsingi zinampa mwananchi fursa ya kutotumia pesa wakati
anapougua kwani akiwa na kadi na NHIF anatibiwa bure.
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa (KGPC), Deogratius Nsokolo, alisema kuwa mfuko huo ni
muhimu sana kwa waandishi wa habari hasa ukizingatia kuwa hufanya kazi katika mazingira magumu na
hatarishi.
“Mara
nyingi huwa tunasafiri hapa na pale katika shughuli yetu ya habari na magonjwa
kwa binadamu huwa hayatoi taarifa, huja tu muda usio tarajia, hivyo kama
unakadi ya NHIF, una fursa ya kupata matibabu popote pale utakapopata matatizo
ya magonjwa” alisema Nsokolo.
Wanahabari
waliojiunga na mfuko huo na kukabidhiwa kadi zao ni pamoja na Deogratius
Nsokoro (ITV),Adela Madyane (Kigoma Yetu),
Fadhir Abdalah (Habari Leo), Mwajabu Kigaza (Majira), Magreth Magoso
(Jambo Leo).