WANASIASA
wa vyama vyote nchini ambao ndio wadau wakubwa wa uchaguzi unaotarajiwa
kufanyika Octoba mwaka huu wametakiwa kutokuwa chanzo cha vurugu na migawanyiko
ya aina yoyote ambayo inaweza kuhatarisha amani ya nchi.
Kauli
hiyo ilitolewa hapo jana na Umoja wa Maaskofu na Wachungaji Mkoani Kigoma katika
Ufunguzi wa mkutano wa Injili unaoendelea katika viwanja vya Community Center
katika Manispaa ya kigoma – Ujiji.
Akisoma
risala kwa niaba ya Maasko na Wachungaji mkoani hapa, Mchungaji wa Kanisa la
Pentecote Assembless Of God Tanzania (PAGT-Katubuka), Michael Kulwa, alisema
kuwa, wanasiasa hawanabudi kujilinda na kauli, lugha na matamshi ili kuufanya
kampeni za uchaguzi na uchaguzi wenyewe kukamilika kwa amani na utulivu.
Kulwa
alisema kuwa, kitendo cha wanasiasa kutokulinda kauli zao kunaweza kusababisha
madhara makubwa na hata umwagikaji wa damu usio na sababu hivyo wote kwa pamoja
wanatakiwa kukumbuka amani ya Tanzania inatakiwa kulindwa kila wanapokuwa
Jukwaani kunadi sera zao.
“Ushauri
wetu sisi Maaskofu na Wachungaji Mkoani Kigoma ni wanasiasa kufuata sheria na
taratibu zilizowekwa ili kuilinda amani ya nchi yetu,” alisema Kulwa.
Aidha
Kulwa alisema kuwa, wao kama Watumishi wa Mungu wanaahidi kuendelea
kushirikiana na serikali pamoja na vyombo vyake vya dola katika kuhakikisha
ambani ya nchi inaendelea kutawala kwa muda wote wa kampeni hadi uchaguzi na
baada ya uchaguzi.
“Pia
tutaendela kuwanyooshea vidole waovu kila iitwapo leo. Kwa kuonya na kukemea
maovu ya kila aina ikiwemo rushwa, wizi wa mali za umma, uzembe kazini na
ukiukwaji wa sheria unaofanywa kwa makusudi” alisisitiza.
Kwa
upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Kanali Mstaafu Issa Machibya, ambaye
alikuwa mgeni rasmi katika mkutano huo, aliwataka wananchi kutokukubaliana na
wanasiasa watakaotaka kuwagawa kwa misingi ya udini na ukabila na wala
wasikubali kutumiwa kwa namna yoyote ile kuleta vurugu.
Machibya
aliema kuwa, ni jukumu la kila mmoja kulinda amani ya nchi sasa kama wananchi
watakubali kutumiwa kuleta vurugu basi watakuwa wanaiingiza nchi yetu katika
machafuko ambayo yanaweza kupelekea umwagaji wa damu.
“Nitoe angalizo kwa wananchi wote kuhusu viongozi
wanaotafuta madaraka kwa kutumia rushwa, hebu tujiulize, huyu atakayepata
madaraka kwa kutoa rushwa, je ataweza kukemea vitendo vya rushwa na ufisadi
pindi atakapokuwa madarakani? Jibu ni hapana” aliongeza Machibya.