WANACHAMA wa Kikundi cha Hisa cha
kina Mama, Masanga Group, kilichoko mtaa wa Masanga katika Manispaa ya Kigoma
Ujiji, wameingia katika mgogoro na viongozi wa kikundi hicho kufuatia kutopewa
pesa zao ambazo walikuwa wakiweka kama hisa na kuwatuhumu viongozi hao kwa
ubadhirifu.
Wakizungumza na Blog hii, kina mama hao wamedai kuwa walipaswa kuvunja hisa na kila mwanachama
kupatiwa mtaji aliowekeza pamoja na faida kwa mujibu wa taratibu tangu mwezi
Agosti mwaka huu, lakini hadi sasa viongozi wao wamekuwa wakiwapa majibu
yasiyoridhisha kuhusu pesa zao.
Baadhi ya akina mama mkoani Kigoma (Picha haihusiani na Habari) |
Katika ofisi ya Polisi Jamii kituo
cha Masanga ambapo akina mama hao walikusanyika kwa ajili ya kutafuta suluhu ya
suala hilo chini ya mwenyekiti wa mtaa, baadhi ya wanachama hao wakiwemo
Dainesi Damian na Mariam Kasunzu , wamepinga kauli ya viongozi wao kuwa pesa
hizo ziko mikononi mwa baadhi ya wanachama waliokopa.
“Madeni yalioko nje ni kama shilingi
million 12 hadi 16 na mitaji ya watu walioweka pesa zao ni zaidi ya Milioni 38,
sasa hapo tunashindwa kuelewa ni kwanini watu wanashindwa kugawiwa pesa zao
nawakati pesa zipo tena zaidi ya milioni 38” amehoji Mariam Kasunzu.
Aidha wanachama hao wamewatuhumu
viongozi wao kwa kukiuka taratibu za uendeshaji wa kikundi hicho kutokana viongozi
kutowapa mikopo wanachama wanaotaka kwa njia harari bali hutoa mikopo kinyume
na taratibu.
“Kawaida sisi tunakopa mkopo kwa
liba ya asilimia 10 lakini ukiomba mkopo wa asilimia 10 kwenye kitabu unaambiwa
hakuna pesa hata kama umeomba shilingi 50,000/=, lakini ukiomba mkopo wa
pembeni wa liba ya asilimia 20 ambazo katibu aliamua kuwakopesha wanawake
wenzake kwa maslahi yake unapewa hata laki tano” amesema Damian
Kwa upande wake Katibu wa Kikundi hicho
cha Hisa, Alijumo Seme, alikanusha tuhuma za ubadhirifu zilizoelekezwa kwao
ambapo alisema hatua zimeanza kuchukuliwa kwa wanachama wenye madeni na tayari
taratibu za kuwafikisha Polisi zinafanyika.
Nae Mwenyekiti wa kikundi hicho,
Salma Sabuhoro, amekiri ukiukwaji wa baadhi ya taratibu za uendeshaji wa
kikundi likiwemo suala la mikopo kitu kilichosababisha wanachama kutoelewana na
viongozi.