KATIKA
kuhakikisha ugonjwa wa Kipindupindu mkoani Kigoma unatokomezwa, Serikali ya
mkoa imesema itafanya zoezi la ukaguzi wa nyumba kwa nyumba kuhusu uwepo na
utumiaji wa vyoo katika Manispaa ya Kigoma Ujiji.
Akizungumza
na wananchi wa Kata ya Kibirizi hapo jana, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma Saveri
Mwangasame amesema kuwa ukaguzi huo utaambatana na kukagua hari ya usafi katika
Manispaa hii.
Mwangasame
alisema kuwa, ofisi yake inatarajia kuendesha operation hiyo kuanzia jumatatu
30 ili hatua ziweze kuchukuliwa dhidi ya familia zitakabainika kutokuwa na vyoo
na wataanzia katika kata ya Kibirizi ambayo inaelezwa kuwa na wagonjwa wa
kipindupindu.
“Sasa
hivi Kigoma kuna ugonjwa wa kipindupindu na bado hatujatangaza rasmi kuwa
kipindupindu kimekwisha hivyo bado tunaendelea kupambana na ugonjwa huo kwa
hatua ya kukagua vyoo kila nyumba” alisema Mwangasame.
Aidha
Mwangasame alisema kuwa katika zoezi hilo endapo kuna nyumba itabainika haina
choo mmiliki wa nyumba atachukuliwa hatua za sheria sambamba na watu ambao
hawatumii vyoo badala yake kwenda kujisaidia ziwani.
“Bado
kuna watu wanaoga na kujisaidia ziwani, katika hili hatutakuwa na utani kabisa
mana mtu akibainika sheria lazima ichukue mkono wake ili iwe fundisho kwa
wengine na katika zoezi la kukagua nyumba hadi nyuma na mimi nitakuwepo ili
kuonyesha tumedhamilia kupambana na hari hiyo” alisisitiza Mwangasame.
Hata
hivyo wakati Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kigoma ikijiandaa kufanya Oparesheni
hiyo, wananchi katika Manispaa hii waliwatupia lawama viongozi wa manispaa hasa
sekta ya afya kwa kushindwa kuzungukia maeneo ya mji ili kuhimiza suala la
usafi.
Shekhe
Jariji Rashid alisema kuwa, utekelezaji wa viongozi wa usafi umelegalega kutokana
na maeneo mengi kuzagaa uchafu na akatolea mfano eneo la stand ya daradara
ambapo baadhi ya madreva hujisaidia nyuma ya magari yao hivyo kusababisha
harufu kuzagaa lakini viongozi wa afya hawalijui hilo kutokana na wao kukaa
maofisini kwao.
Nae
Issa Kalumanzira alisema kuwa, licha ya kuwa viongozi wa Manispaa wanahimiza
usafi ila na wao si wasafi kutokana na Zahanati ya Kibirizi ambacho kimetengwa
kwaajiri ya wagonjwa wa kipindupindu ila usafi katika vyoo vya zahanati ile ni
vichafu.
“Tungetegemea
kuwa zahanati ile ndio ingekuwa safi ili kuzuia kipindupindu kuenea kwa watu
wengine ila cha ajabu viongozi hawajari hari mbaya ya uchafu katika vyoo na
maeneo mengine na sasahivi wanatwambia watatukagua wakati wao wenyewe
hawajikagui” alisema Kalumanzira
Hata
hivyo wananchi hao wameitaka Manispaa kuacha kuwatupia lawama wananchi mana
hata wao zoezi la uondoaji taka katika madampo yasiyo rasmi kwa muda mwafaka linaonekana kuwashinda hivyo
walekebishe tatizo hilo kwanza mana nalo ni chanzo cha Kipindupindu.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Manispaa ya Kigoma Ujiji Boniface Nyambelea amezungumzia
suala hilo la uzoaji taka kushindwa kufanyika kwa kiwango kizuri ambapo alisema
kuwa changamoto inayosababisha ni kukosekana kwa vitendea kazi vya kutosha kama
magari kwani mji mzima unategemea magari mawili tena ya kukodi.