Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma, Naibu Kamishina Maurice Kitinusa. |
Jumla ya wakimbizi 130,041 wameingia nchini
wakitokea nchi jirani ya Burundi kwa lengo la kutafuta hifadhi baada ya kutokea
kwa machafuko nchini kwao mapema mwaka jana 2015.
Akizungumza
na blog hili hapo jana, Afisa uhamiaji Mkoa wa Kigoma, Naibu Kamishina Mourice
Kitinusa, alisema kuwa idadi hiyo ni kuanzia Aprili mwaka jana ambapo wakimbizi
hao hupelekwa katika kambi tatu tofauti kwaajiri ya hifadhi.
Alisema
kuwa, Mkoa huu una kambi tatu za wakimbizi ikiwemo kambi ya Nyarugusu iliyoko
Wilaya ya Kasulu yenye wakimbizi 86,434, Nduta Wilayani Kibondo yenye wakimbizi
41,572 na kambi mpya ya Mtendeli ambayo ina watu 1596.
“Idadi
hiyo ni wale ambao wanaingia moja kwa moja kwenye makambi ila wapo ambao
hawapiti katika vituo rasmi mana kunapotokea machafuko mtu hukimbilia popote
hivyo wengine huingia vijijini na kujisalimisha
kwa viongozi wa vijiji ili kuomba
hifadhi” alisema Kitinusa.
Kitinusa
aliongeza kuwa, wakimbizi waliokuwa wakiomba hifadhi mpaka sasa ni 439 hivyo
wanasubiria taratibu zifanywe na UNHCR
ili kuwasafirisha makambini ili kuwapatia hifadhi.
Aidha
Kitinusa alisema kuwa, kutokana na wakimbizi wengine kushindwa kupitia katika
maeneo yaliyotengwa na serikali na kujikuta wakiingia moja kwa moja vijijini, viongozi
wa vijiji wanatakiwa kuwachukua na kuwakabidhi katika ofisi za uhamiaji.
“Kupitia
suala hilo sasa viongozi wa vijiji tunawaomba watoe ushirikiano kwa kuwapokea wakimbizi wanaofika katika
maeneo yao na kuwakabidhi katika ofisi za uhamiaji pia kwa wale ambao huwa
hawajisalimishi basi wawakamate mana ni makosa kukaa na mkimbizi katika eneo
lako.
“Pia
kwa wanavijiji nao wanatakiwa kutoa ushirikiano pale wanapokutana na wakimbizi
basi watoe taarifa kwa viongozi wao badala ya kuwaacha, ifahamike kuwa kutoa
taarifa kuhusu uwepo wa wakimbizi katika maeneo yao si makosa bali makosa ni
kukaa na wakimbizi bila kutoa taarifa na watu wanaofanya hivyo wakikamatwa hatua
za kisheria huchukuliwa dhidi yao” alisema Kitinusa.
Hata
hivyo inadaiwa kuwepo kwa ongezeko kubwa la wakimbizi kutoka nchini Burundi
wanaoingia nchini kwa lengo la kuomba hifadhi kutokana na machafuko ya kisiasa yanayoendelea nchini
kwao.