Kigoma Online News

FURNITURE

KALIHAMWE STATIONARY

KALIHAMWE STATIONARY

Feb 11, 2016

SERA YA UTOAJI ELIMU BURE WAIBUA VIKWAZO MASHULENI

Kaimu Afisa Elimu wa Mkoa wa Kigoma, Venance Babukege. 





Baada  ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania John Magufuri kuagiza elimu itolewe bure suala hilo limeibua changamoto ya ukosefu wa madawati katika baadhi ya shule za msingi mkoani Kigoma.

Akizungumza na hivi karibuni, Mwalimu Mkuu wa shule ya Msingi Majengo, Octavian Lazaro alisema kuwa, shule yake inakabiliwa na uhaba wa madawati kutoka na wingi wa wa watoto waliokuja kuandikishwa shuleni hapo.

Lazaro alisema kuwa, mpaka sasa zaidi ya wanafunzi 170 wanakaa chini huku wazazi wakiendelea kuleta watoto wao ili kuanza masomo.

Aidha Lazaro alisema kuwa,  ongezeko la wanafunzi hauendani na uwiano wa huduma bora kwakuwa shule ina wanafunzi 1060 wakati madawati yaliyopo ni 180 na ndio yanatumiwa na wanafunzi wa kuanzia darasa la awali hadi darasa la saba.

"Kwa idadi hiyo sasa wanafunzi 173 wanakaa chini na ili kutatua tatizo la watoto kukaa chini, shule inahitaji madawati 353" Aliongeza Lazaro.

Alisema kuwa, kama serikali inahitaji kuendelea kutoa elimu bure kwa wanafunzi na kufanikiwa katika hilo, inatakiwa pia kutatua changamoto zinazojitokeza wakati wa kutekeleza agizo hilo na kufanikiwa.

“Mahitaji yanazidi kuongeza naiomba serikali itatue changamoto ya madawati sambamba na kuongeza matundu ya vyoo ambayo yanaonekena Kuwa machache kulingana na idadi ya wanafunzi waliopo.

"Shule ina matundu ya vyoo 6 tu, na inahitajika kupatikana matundu 49 ambayo yatasaidia wanafunzi 20 kutumia tundu moja la choo hivyo kuondoa usumbufu na madhara yanayoweza kusababishwa na uchache wa matundu ya vyoo " alisema Lazaro.

Hata hivyo Lazaro aliitaka idara ya elimu mkoa hapa izingatie uwiano wa walimu kwa kuzingatia Mahitaji ya shule kutokana na baadhi ya shule kuwa na walimu wachache huku wanafunzi wakiwa wengi pia kuongeza madarasa katika shule ambazo zina madarasa machache.

Sambamba na shule hiyo, shule nyingine inayokabiliwa na uhaba wa madawa ni shule ya msingi Airport ambapo kati ya wanafuzi 1490 waliopo shuleni hapo, wanafunzi 1269 wanakaa chini huku shule ikiwa na madawati  221 pekee na kila chumba cha darasa kina zaidi ya wanafunzi 200.

Kwa mujibu wa baadhi ya Walimu shuleni hapo ambao hawakutaka majina yao kutajwa, walisema Kuwa, changamoto ya madawati katika shule hiyo ni ya muda mrefu na licha ya viongozi wa elimu kufahamu lakini hakuna utekelezaji unaofanyika.

Akijibu kuhusu kero ya madawati, Kaimu Afisa Elimu wa Mkoa wa Kigoma, Venance Babukege alisema kuwa, suala la madawati linashughulikiwa na Halmashauri na maelekezo ya serikali kwa wakuu wa Wilaya wote nchini ni kwamba ifikapo Juni 30 asiwepo mwanafunzi anaekaa chini.

"Kwa maana ya mkoa, Mkuu wa Mkoa ameweka lengo lake kuhakikisha suala hilo linakamilika ndani ya miezi mitatu na kwenye kikao cha RCC tuliazimia hivyo " alisema Babukege

Babukege aliongeza kuwa, kuhusu miundombinu shuleni kama vyoo na madarasa ni jukumu la wazazi hiyo ni kwamujibu wa ugharimiaji wa elimu bure ambapo serikali itasaidia pale watakapokuwa wamefikia.

" Serikali haiwezi kugharimia elimu na kujenga miundombinu ila wananchi wanatakiwa watekeleze miundombinu halafu kazi ya serikali ni kuhakikisha inatimiza gharama zote za elimu shuleni "alisema Babukege.