Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma, Naibu Kamishina Maurice Kitinusa. |
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Afisa Uhamiaji Mkoa wa Kigoma, Naibu Kamisha, Mourice Kitinusa alisema kuwa, wahamiaji hao walikamatwa Februari 9 mwaka huu majira ya saa 9:00 usiku baada kufanya msako.
Kitinusa alisema kuwa, wengi wa wahamiaji hao ni kutoka nchini Burundi na wanatumiwa katika shughuli za kilimo cha tumbaku na migodi ya chokaa, ambapo watanzania ndio wanaowaajiri.
"Watanzania wengi wanajisahau Kuwa kuwatumikisha wahamiaji bila vibali ni kukiuka sheria za nchi mana Kama unawatumikisha huku wakijua huna kibali inakuwa rahisi kwao kufanya uharifu ndio mana wamo watanzania tuliowakamata "alisema Kitinusa.
Aidha Kitinusa aliongeza Kuwa, kwa kipindi cha Januari walikamata wahamiaji 326 na Februari 9 walikamata wahamiaji 51 ikiwa ni jumla ya wahamiaji 377 waliokamatwa kipindi cha Januari na Februari.
"Wahamiaji hawa tuliowakamata ni wakimbizi kutoka katika kambi zilizofungwa na waliorudishwa kwao mwaka jana na wengine ni wale wanaoishi kinyemela baada ya vibali kuisha muda wake"aliongeza Kitinusa.
Kwa upande wake Kaimu mtendaji wa Kijiji cha Mazungwe, Mwalimu Primo Kiwike, aliishauri idara ya uhamiaji kutumia lugha nyepesi wanapowahoji raia mana maafisa wengi hutumia lugha za vitisho jambo linalofanya wananchi waogope hata kama ni watanzania.
"Mimi pia ni mwalimu wa shule ya msingi Mazungwe, kati ya 51 waliokamatwa tisa ni watanzania japokuwa kijiji tumewawekea dhamana, ila kukamatwa kwao kunatokana na lugha wanazotumia maafisa uhamiaji ambazo zinawafanya washindwe kujieleza vizuri "alisema Kiwike