Kigoma Online News

FURNITURE

KALIHAMWE STATIONARY

KALIHAMWE STATIONARY

Apr 8, 2017

KAYA MASIKINI KIGOMA ZANUFAIKA NA MRADI WA TASAF

Wananchi wanaonufaika na mradi wa TASAF awamu ya tatu katika Manispaa ya Kigoma Ujiji wamesema mradi huo umewasaidia kutatua changamoto ya elimu na afya katika familia zao huku wengine wakianzisha miradi ya maendeleo kupitia fedha wanazopewa.

Wakiongea kwa niaba ya wananchi wengine wanaonufaika na mradi huo, Bi Mwajuma Ramadhani, Bi Rose Nteza na Athumani Jumanne wamesema awali walikuwa wakipata shida katika kukabiliana na mahitaji ya watoto wao hasa kinapofika kipindi cha kufungua shule jambo lililokuwa likiwafanya washindwe kwenda shule.

Wamesema kuwa, kwasasa wanatumia pesa wanazopewa na TASAF kuwanunulia sare za shule watoto wao pamoja na vitabu jambo linalofanya utoro mashuleni kupungua huku maendeleo yao shuleni kuwa mazuri.

Aidha, wamezungumzia suala la afya kwa kusema kuwa kwasasa wanahudhuria hospitali kila wanapopata magonjwa hasa akina mama wajawazito na watoto wanaotakiwa kufikishwa kliniki huku wakibainisha kuwa wengi wao wamejiunga na mfuko wa matibabu wa tika unaowasaidia kupata matibabu bure.

“Kwakweli tunaishukuru TASAF kwa msaada wanaotupa mana wengine tumenunua mifugo kama kuku na mbuzi ili zitusaidie katika maisha na wengine wameanza akufanya biashara ndogondogo ili kuzungusha pesa wanazopewa,” walisema.

Kwa upande wake Mratibu wa TASAF Manispaa ya Kigoma Ujiji, Robert Saboya amesema  kaya 10,247 zinanufaika na mradi huo kutoka katika mitaa 49 iliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji tangu Tasaf awamu ya tatu ianze.

Ameongeza kuwa  lengo kubwa la mradi wa  huo  ni kujenga rasilimali watu hususa ni watoto wanaokwenda shule na wanaohudhuria kliniki huku akibainisha changamoto  zinazowakabili kuwa ni jinsi ya  kukusanya data za wanafunzi na watoto.