Taasisi ya Mo Dewji imekuwa miongoni mwa wadhamini ambao kwa
kushirikiana na Taasisi ya Tulia Trust wamewezesha kufanyika Tulia Marathon
2018, ikiwa ni mara ya pili kufanya hivyo baada ya mbio za mwaka jana ambazo
zilikuwa na mafanikio makubwa.
Akizungumza katika mbio hizo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla alisema watu wengi
hawana utaratibu wa kufanya mazoezi jambo ambalo sio zuri kiafya na hivyo kuwataka
wananchi kufanya mazoezi ili kuimarisha afya zao.
Aidha Makalla alimpongeza
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Mwanzilishi wa Taasisi ya Tulia Trust, Dkt.
Tulia Ackson kwa kuanzisha mbio hizo ambazo zinasaidia sana mkoa huo kuboresha
sekta ya afya na elimu.
“Michezo ni muhimu sana kwa afya zetu … tujifunze na sisi tuanze kufanya
mazoezi sababu ni muhimu sana kwa afya zetu. Mimi hapa nilipo sijawahi kuumwa
maralia tangu nikiwa kidato cha kwanza lakini sababu nafanya mazoezi. Ukiwa
unafanya mazoezi magonjwa haya ya pressure unaachana nayo,” alisema na
kuongeza.
“Niseme tunafaidika sana kupitia Trulia Trust kwa mambo ambayo
anayafanya, anaupenda mkoa wetu ameboresha miundombinu katika elimu na afya. Alianza
kwenye ngoma na sasa anafanya Tulia Marathon na kutokana na marathon hii anakwenda
kusaidia afya na elimu.”
Naye Meneja Miradi wa Taasisi ya Mo Dewji, Rachel Chengula alisema
wameamua kushirikiana na Tulia Trust ili kusaidia kuokoa maisha ya Watanzania
ambao wamekuwa wakipoteza maisha kutokana na kukosa huduma bora za afya.
“Tunatambua kwamba maisha ya mwanadamu yanaanza mimba inapotungwa hivyo
ni muhimu sisi kama sehemu Watanzania tuliojengwa katika misingi ya upendo
kuona ni muhimu kushirikiana na serikali na wadau wengine kama Tulia Trust kuweka
mazingira bora ya wodi za uzazi ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi nchini,
“Tunapongeza hatua ambazo zinachukuliwa na serikali za kukarabati vituo
vya afya katika
Halmashauri mbalimbali nchini kwa kujenga na kukarabati majengo ya upasuaji,
wodi za wazazi na watoto pamoja na maabara.
Tunaamini jitihada hizi zitasaidia kupunguza vifo vya kina mama na watoto
nchini,” alisema Chengula.
Awali akizungumza kuhusu Tulia Marathon 2018,
Dkt. Tulia alisema fedha ambazo zimepatikana katika mbio za mwaka huu
zitatumika kusaidia kuboresha sekta ya elimu na afya kama ilivyokuwa mwaka jana
na lengo lao ni kushirikiana na serikali ili kuwezesha wananchi wapate huduma
bora za kiafya na elimu bora.
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Mwanzilishi wa Taasisi ya Tulia Trust, Dkt. Tulia Ackson akiongoza wanariadha waliojitokeza kukimbia katika Tulia Marathon 2018 zilizofanyika Jijini Mbeya.
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Mwanzilishi wa Taasisi ya Tulia Trust, Dkt. Tulia Ackson akielezea mafanikio ambayo Tulia Marathon iliyapata kwa mwaka uliopita na mipango ya mwaka huu.
Meneja Miradi wa Taasisi ya Mo Dewji, Rachel Chengula akizungumza kuhusu Tulia Marathon 2018 na shughuli ambazo taasisi yao inafanya kwa jamii. Kulia kwake ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania ambaye pia ni Mwanzilishi wa Taasisi ya Tulia Trust, Dkt. Tulia Ackson.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amos Makalla akizungumza namna Tulia Marathon inawasaidia kuboresha sekta ya afya na elimu na kutoa pongezi kwa Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson.
Meneja Miradi wa Taasisi wa Mo Dewji, Rachel Chengula akikabidhi medali na fedha taslimu kwa washindi wa mbio za 5 KM zilizohusisha wanafunzi katika Tulia Marathon 2018 zilizofanyika Jijini Mbeya.