JESHI
la Polisi mkoani Kigoma limefanikiwa kukamata nyara za serikali zenye thamani
ya Tsh. 37,625,000/=, kwenye maeneo ya Hifadhi ya Gombe kijiji cha Mgambazi
wilaya ya Uvinza mkoani hapa.
Akizungumza
na waandhishi wa habari hapo jana, Kamanda wa Polisi mkoani Kigoma, SACP
Ferdinand Mtui, alisema kuwa, tukio hilo lilitokea Julai 13 majira ya saa 7: 00
mchana wakati Askari Polisi wakiwa kwenye msako kwa kushirikiana na Askali wa
Hifadhi ya Gombe.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoa SACP Ferdinand Mtui |
Kamanda
Mtui alisema kuwa, Nyara hizo zilikamatwa nyumbani kwa Jackson Evarist (44)
mkazi wa Mgambazi baada ya Polisi kufanya upekuzi nyumbani kwake kufuatia taarifa
za Kiintelijensia kuhusu umilikaji wa nyara hizo kinyume cha sheria.
“Nyara
zilizopatikana nyumbani kwa Jackson ni
pamoja na meno sita ya tembo yenye uzito wa kg 28 na thamani ya Tsh.
30,100,000/=, ngozi na fuvu moja la chui vyenye thamani ya Tsh.7,525,000/= .
“Nyara
zote zilikuwa zimehifadhiwa katika mfuko
wa sandarusi uliokuwa ndani ya chumba cha kulala mtuhumiwa” alisema Kamanda Mtui.
Aidha
Kamanda Mtui alisema kuwa, Upekuzi huo ulifanyika chini ya uangalizi wa Viongozi
wa serikali ya Kijiji na Mtuhumiwa atafikishwa mahakamani mara baada ya
upelelezi kukamilika.
Sambamba
na kuwashukuru wananchi kwa taarifa walizotoa zilizopelekea kukamatwa kwa nyara
hizo, Kamanda Mtui aliwataka wananchi mkoani hapa kutokuchoka kushirikiana na
Jeshi la Polisi katika kufichua vitendo
vya uharifu na waharifu.
Mwisho.