Kigoma Online News

FURNITURE

KALIHAMWE STATIONARY

KALIHAMWE STATIONARY

Dec 21, 2015

KIWANGO CHA UFAULU KIGOMA CHAPANDA



KIWANGO cha Elimu ya Msingi mkoani Kigoma kimeonekana kupanda kwa mwaka huu 2015 ukilinganisha na  mwaka jana baada ya ufauru wa wanafunzi wa walimaliza  darasa la saba mwaka huu kupanda kwa asilimia 12.01.

Akizungumza katika hafra ya upangaji matokeo ya darasa la saba mwaka 2015 mkoani hapa mwishoni mwa wiki iliyopita , Kaimu Afisa Elimu wa mkoa wa Kigoma, Venance Babukege, alisema kuwa matokeo ya mwaka huu ni mazuri ukilinganisha na matokeo ya mwaka jana.
Kaimu Afisa Elimu wa mkoa wa Kigoma, Venance Babukege, akizungumza katika hafra ya upangaji matokeo ya darasa la saba mwaka 2015 mkoani humo mwishoni mwa wiki iliyopita, kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kanali Mstaafu Issa Machibya .
Alisema kuwa, ufauru wa wanafunzi waliomaliza darasa la saba mwaka huu ni asilimia 54.04% wakati mwaka jana ilikuwa 42.025%  hivyo ufaulu wa mwaka huu ukipanda kwa asilimia 12.01.

Aidha Babukege alisema kuwa, kuongezeka kwa ufaulu mwaka huu kunasababishwa na walimu kutimiza wajibu wao pamoja na wazazi kuhimiza mahudhurio ya lazima kwa watoto wao pia serikali kutoa  vitendea kazi mashuleni kwa wakati sambamba na kuhamasisha walimu katika ufundishaji.

Babukege alisema kuwa, baada ya mwaka jana ufaulu kuwa wa kiwango cha chini waliweka mipango mikakati ya kimkoa ili kuinua elimu na walikuwa wakiwachukulia hatua walimu ambao ni wazembe kutimiza wajibu wao.
Kaimu Afisa Elimu wa mkoa wa Kigoma, Venance Babukege, akizungumza katika hafra ya upangaji matokeo ya darasa la saba mwaka 2015 mkoani humo mwishoni mwa wiki iliyopita, kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kanali Mstaafu Issa Machibya .
 “Mwaka huu  tulifukuza walimu 12  kutokana na utoro na kutokufundisha darasani hivyo ili kuendana na kasi hii ya kuinua elimu  tutaendelea kuwachukulia hatua kali za kinidhani ikiwa ni pamoja na kufukuzwa kazi  walimu ambao watawaacha wanafunzi darasani  huku wao wakiendelea na shughuri zao  nje ya ufundishaji” alisema Babukege.

Aliongeza kuwa, kila shule katika Wilaya zote mkoani hapa zimefanya vizuri huku Wilaya ya Kigoma Mjini ikiwa ya kwanza kwa ufaulu kimkoa ambayo ina asilimia 64 wakati wilaya ya Kakonko ikiwa ni ya mwisho yenye asilimia 48.

“Kwa upande wa Shule zilizoongoza, shule iliyoongoza kimkoa ni  Mwiramvya ambayo ni shule ya mchepuo wa kiingereza  na katika kumi bora ya wanafunzi waliongoza kimkoa wote wametoka katika shule hiyo, shule ya pili ni Mtondo na shule ya Boma ya Kibondo ikiwa ni ya tatu” alisema Babukege.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma Eng. John Ndungulu, akizungumza katika hafra ya upangaji matokeo ya darasa la saba mwaka 2015 mkoani humo mwishoni mwa wiki iliyopita, kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Kanali Mstaafu Issa Machibya .
 Kwa upande wake, Afisa Elimu wa Wilaya ya Uvinza Idara ya Elimu Msingi, Mwl. Frank Magagiro ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mtendaji katika kikao hicho, alisema kuwa, sababu mojawapo iliyochangia kuongezeka kwa ufaulu mwaka huu ni kuongezeka kwa waalimu baada ya kupata mgao kutoka TAMISEMI.

Alisema kuwa, mwaka jana ufaulu ulikuwa duni kutokana na upungufu mkubwa wa walimu kwani baadhi ya shule zilikuwa na walimu wawili hadi watatu pia kukiwa na changamoto ya miundombinu ya vyumba vya madarasa na madawati.

“Kuna shule zilikuwa na  chumba kimoja cha darasa na zingine zikiwa na vyumba viwili au vitatu  hivyo serikali inaendelea kujipanga katika  mwaka huu wa fedha 2016/2017 tunatarajia kuongeza vyumba vya madarasa katika shule zenye upungufu sambamba na kuwahamasisha wazazi kuhusu utoro wa wanafunzi” alisema Magagiro