Kigoma Online News

FURNITURE

KALIHAMWE STATIONARY

KALIHAMWE STATIONARY

Dec 22, 2015

MADIWANI WA HALMASHAURI YA WILAYA YA KIGOMA WATAKIWA KUSHIRIKIANA NA WANANCHI


Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma wametakiwa kushirikiana na wananchi  pamoja na watumishi  ili kuhakikisha wanaleta maendeleo katika kata zao na halmashauri kwa ujumla.

Akizungumza katika kikao cha kwanza cha madiwani wa Halmashauri hii, Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Saveli Mwangasame, alisema kuwa ushirikiano ni chanzo cha mafanikio katika maeneo yoyote yale hivyo ili  kuleta maendeleo katika kipindi hiki cha miaka mitano suala la ushirikiano linatakiwa kupewa kipaumbele na kuachana na itikadi za kivyama.
Mkuu wa Wilaya ya Kigoma, Saveli Mwangasame, akizungumza na madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma mwishoni mwa wiki iliyopita.
Alisema kuwa, madiwani peke yao hawawezi kutimiza suala la maendeleo ndio mana serikali iliweka watumishi katika Halmashauri ili watoe ushirikiano kwa madiwani katika kusimamia maendeleo.

Aidha Mwangasame alisema kuwa, kuna sekta nyingi ambazo zinaweza kuingiza kipato katika Halmashauri ikiwemo uvuvi ndani ya Ziwa Tanganyika, kodi na Shughuri mbalimbali za uzalishaji ambazo zote zinaweza kuongeza kipato cha halmashauri ambacho kitasaidia katika utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo.

Mwangasame aliwataka madiwani hao kusimamie shughuri zote ambazo zinaingiza kipato cha Halmashauri  na kuwa msitari wa mbele kupambana na uvuvi haramu katika Ziwa Tanganyika ambao ni chanzo cha kudhoofisha mapato katika Halmashauri hii.
Mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, Enock Jonas, akizungumza na madiwani baada ya kuchaguliwa katika kikao chao cha kwanza.
 “Wananchi waliwaamini ndio mana waliwachagua hivyo ninaimani watatoa ushirikiano wa hari ya juu kwenu katika kutekeleza masuala ya kimaendeleo, cha msingi ni kuwa na umoja baina yenu madiwani, watumishi wa Halmashauri na wananchi” alisema Mwangasame.

Nae Mwenyekiti wa Mpya wa  Halmashauri hiyo, Enock Jonas, alisema kuwa, madiwani wote wana vyama vyao ila kampeni zilishapita hivyo kwasasa ni kipindi cha kufanya kazi kwa ushirikiano ili kurudisha imani kwa wananchi waliowachagua.

Alisema kuwa, ili kuleta maendeleo katika Halmashauri tunatakiwa kuweka kado tofauti za midini, kikabila na kikanda ili kufanya kazi kwa pamoja na kuangalia maslahi ya wananchi badala ya kuangalia maslahi ya mtu mmoja.

“Hii Halmashauri ni yetu tukishindwa kuiendeleza tutazomewa na wale tulio washinda na katika uchaguzi ujao wananchi hawatotuamini tena, mimi kama Mwenyekiti nitasimamia sharia na nitatoa ushirikiano kwa kila diwani” alisema Jonas.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hii, Gwami John, alisema kuwa, imani yake ni kwamba ushirikiano utakaojengwa baina ya madiwani, watumishi wa halmashauri, wakuu wa idara pamoja na wananchi utakuwa chachu ya kuleta maendelo.

Hata hivyo John aliwataka wakuu wa idara kuwajari wananchi kwa kuwatatulia matatizo yao wakati wanapofika katika ofisi zao badala ya kuwasumbua kwa sababu zisizo za msingi jambo ambalo lilikuwa likipigiwa kelele na wananchi.

“Kumekuwa na tabia kwa baadhi ya wakuu wa idara kuwasumbua wananchi kwa kuwaambia waje kesho hata kama tatizo lao linaweza kutatuliwa muda huohuo, tukumbuke kuwa mwananchi huyo anatumia nauli, pesa ya malazi na hata chakula sasa unapokuwa unamwambia njoo kesho unamfanya apoteze pesa zake wakati ungeweza kumuhudumia haraka” alisema John.