MADIWANI
wa Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma wametakiwa kujiunga na Mfuko
wa Bima ya Afya (NHIF) ili wawe na uhakika wa matibabu pindi wanapougua wao na
wategemezi wao.
Akizungumza
katika kikao cha kwanza cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo hapo jana, Meneja
wa NHIF mkoani Kigoma, Elias Odhiambo,
alisema kuwa, kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2009 kufungu cha 3 kila diwani
anapaswa kuwa mwanachama wa mfuko huo.
Alisema
kuwa, ni wazi kuwa kila mtu ni mgonjwa mtarajiwa na ugonjwa unapokuja
hautoi taarifa hivyo mtu anaweza kuugua kipindi ambacho hana pesa
ila kama ameshakuwa mwanachama wa mfuko huo atapata matibabu kwa kutumia kadi ya
uanachama bila kulipa pesa yoyote.
Odhiambo
aliongeza kuwa, ni vyema kwa madiwani hao kujiunga na mfuko huo ili kuwa na uhakika wa matibabu Pia alisema kuwa
kwa watakao hitaji kujiunga watatakiwa
kujaza fomu maalumu kwaajili ya vitambulisho vya matibabu.
''Tutawaleteeni
fomu za kujaza kwaajili ya vitambulisho kwa wale madiwani wapya ila wale
wazamani mtaleta tu vitambulisho vyenu tuwabadilishie kwakuwa nyie hamna haja
ya kujaza fomu tena” alisema Odhiambo.
Naye
Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Mrisho Gambo alisema kuwa, bado katika Wilaya hiyo hali ya mwitikio wa wananchi kujiunga na bima
ya afya ni ndogo ambapo mpaka sasa kuna asilimia 16 tu ya watu waliojiunga.
“Kwanza
madiwani mnatakiwa kuchangamkia fursa kwa kujiunga na mfuko huu na baada ya
hapo kuanza kuwahamasisha wananchi nao wajiunge ili itakapofika mwaka 2017 iwe
imefika asilimia 80 katika Wilaya hii” alisema Gambo.