MAMLAKA
ya chakula, dawa na vipodozi nchini (TFDA) imekamata na kuteketeza kwa moto
tani tatu za bidhaa mbalimbali mkoani Kigoma ikiwemo vipodozi, dawa za binaadam
na mifugo na vyakula vyenye thamani ya shilingili milioni nane na nusu ambavyo
vimepigwa mafuruku na vingine muda wake wa kuuzwa umeisha.
Zoezi
la uchomaji moto wa bidhaa hizo
ulifanyika katika dampo la Lusimbi Manispaa ya Kigoma –Ujiji mkoani hapa kwa
kusimamiwa na Meneja wa TFDA kanda ya Magharibi, Dk. Edger Mahundi.
Akizungumzia
tukio hilo wakati wa kuteketeza bidhaa
hizo, Dk. Mahundi alisema kuwa, bidhaa hizo walizikamata maeneo mbalimbali mkoani
hapa kutokana na msako waliofanya kwa kushitukiza na kufanikiwa kukamata bidhaa
mbalimbali zilizopigwa marufuku na zile zilizoisha muda wake.
Alisema
kuwa, bidhaa hizo walizikamata kwa kushirikiana na maofisa kutoka kanda hiyo ya
magharibi pamoja na wenzao waliopo mkoani hapa na aliwataka wamiliki wa
maduka kufuata sheria za (TFDA) ambapo bidhaa zikiisha muda wake wawe
wanaziondoa wenyewe dukani na kwenda kuziteketeza kwa moto.
“Zoezi
hilo la msako wa kusaka bidhaa feki na zisizofaa kwa watumiaji niendelevu na
litakuwa la kushtukiza kwa Mkoa wa Kigoma hivyo wafanyabiashara ni vyema muwe
waaminifu” alisema Dk. Mahundi.
Naye
Ofisa Afya wa bandari ya mkoa wa Kigoma na Mkaguzi wa mipaka, Theodory
Rutahindurwa, alisema kuwa, wafanyabiashara wasiowaaminifu wamekuwa
wakipitisha bidhaa nyingi ambazo ni feki kwa njia ambazo siyo za halali
jambo ambalo huhatarisha maisha ya watumiaji.
“Wito
wangu kwa wafanyabiashara ni kutii
sheria zilizowekwa na kwa wafanyabiashara watakaobainika na kukutwa na makosa
hayo tena watafungiwa leseni zao sambamba na kufikishwa mahakamani” alisema
Rutahindurwa.