IMEGUNDULIKA kuwa suala la umasikini unaowakabili baadhi ya wakazi mkoani Kigoma umekuwa chanzo cha kudumaza elimu na hivyo
kupelekea baadhi ya Wanafunzi kukatisha masomo na kukimbilia mikoani kufanya
kazi za kuajiriwa.
Hayo yamesemwa na Mkazi wa Kijiji cha Kiganza, Kata ya
Mwandiga katika Wilaya ya Kigoma mkoani hapa, Ashura Kassim alipokuwa anatoa
maoni yake kuhusu changamoto ya baadhi ya Wanafunzi kuacha masomo na kukimbilia
mijini kwa kisingizio cha kutafuta maisha.
Alisema hali ya maisha kwa baadhi ya Watu ni mbaya kiasi
kwamba ni jambo la kawaida kukuta Mwanafunzi anakwenda Shule kusoma bila kuvaa
viatu, sare zimechanika na hana uhakika wa kula chakula pindi anaporudi
nyumbani baada ya muda wa masomo.
“Umasikini wa kipato
umekuwa chanzo cha Watoto wetu kuacha Shule na kwenda Mjini kufanya kazi za
ndani, kuuza maji na kahawa, wengine kukata nyasi za kulisha Ng’ombe na wapo
wanaotiimkia mikoani kufanya kazi za ajab ajabu, hiyo yote chanzo chake ni
Wazazi kukosa fedha za kununua
sare za Shule au viatu.” Alisema Kassim
Aliongeza kuwa inapotokea Mwanafunzi anavaa nguo zenye
viraka humfanya akose raha shuleni kutokana na utani na maneno ya kejeli
anayopata kutoka kwa Wanafunzi wenzake, jambo linalowafanya baadhi kuamua kukatisha
masomo na kukimbilia mjini kutafuta kazi licha ya umri mdogo wanaokuwa nao.
“Ipo haja ya Serikali kuhakikisha inajenga mazingira mazuri
kwa Wananchi ili waweze kumudu kujiajiri wenyewe na hivyo kupunguza utegemezi
katika Familia, kiasi kwamba Watoto wataona fahari kubaki na Familia zao hata
kama hali ya kipato haitakuwa nzuri." Alifafanua zaidi.
Aidha Kassim alishauri kuwa Serikali ijaribu kutengeneza mitaala yenye
mwelekeo wa kuwaandaa Wanafunzi kujiajiri baada ya masomo badala ya hali ilivyo
sasa ambapo kila muhitimu katika ngazi mbalimbali za masomo anajiandaa
kisaikolojia kuajiriwa na Serikali pindi anapomaliza masomo.
Kwa upande wake Sikudhani Amrani, Mkazi wa Kijiji cha Bitale
katika Wilaya ya Kigoma mkoani hapa alisema ipo haja ya Serikali kuboresha
miundombinu ya elimu mkoani Kigoma ili kuwafanya Watoto kupenda masomo ya kila
siku darasani.
“Mazingira mabaya ya Shule zetu yanawafanya baadhi ya
Wanafunzi kuacha Shule na kukimbilia mikoani kutafuta maisha, wanakosa mapenzi
ya kusoma na hata Walimu wao wanajiona kama Watu wasio na thamani kutokana na
hali mbaya ya Shule zao.” Alisema Sikudhani.
Hali ya miundombinu ya Majengo ya Madarasa katika baadhi ya
Shule za Msingi mkoani Kigoma sio ya kuridhisha kutokana na uchakavu, lakini
pia kuna uhaba wa madawati kiasi cha baadhi ya Wanafunzi kukaa chini kwenye
sakafu.