Vyeti feki vikiwa tayari kwaajiri ya kugawiwa kwa wahusika |
Watu watano akiwemo askari mmoja wa
Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani
Kigoma kwa tuhuma za kutengeneza vyeti
bandia vya kitaaluma, miongoni mwake vikiwemo 90 vya uuguzi, ambavyo vilikutwa
vikisubiri kugawiwa kwa wahusika.
Akizungumza na waandishi wa habari
mapema wiki hii, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Naibu Kamishina Ferdinand
Mtui alisema kuwa pamoja na vyeti hivyo vya uuguzi vilivyokamatwa, pia katika
operesheni hiyo walikamata vyeti 37 vya wataalamu wa maabara na vyeti tisa vya
ufamasia.
“Operesheni hiyo ilifanywa kwa pamoja na
maofisa kutoka Baraza la Wafamasia nchini, walikamata jumla ya vyeti 936 vikiwa
kwenye hatua ya ukamilishaji vikiwa bado havijaandikwa majina, miongoni mwake
vikiwemo vyeti 667 vya wauguzi wasaidizi, vyeti 126 vya wataalam wa maabara,
cheti kimoja cha mafunzo ya afya ya jamii na vyeti viwili vya utoaji huduma ya
kwanza” alisema.
Katika kuhakikisha wanakuwa na
uthibitisho wa tuhuma hizo, Kamanda Mtui alisema kuwa pia wamekamata mihuri 25
ya taasisi mbalimbali ikiwemo nyundo mbili, ambazo hutumika kutengenezea mihuri
mbalimbali ya moto.
Aidha Kamanda Mtui aliwataja watu
waliokamatwa katika operesheni hiyo ambayo inahusisha mtandao wa watu
mbalimbali kuwa ni askari wa JWTZ, Mgeni Nyamubozi ambaye ni mume wa mmiliki wa
Duka la Vifaa vya Ofisi la Upendo, lililopo Mwanga mjini Kigoma, ambalo
linatuhumiwa kuhusika na utengenezaji wa vyeti hivyo.
Katika duka hilo, Kamanda huyo wa
polisi alisema polisi walikamata kompyuta mpakato moja, ikiwa na nakala za
vyeti mbalimbali za vyuo na idara za serikali.
Mwingine aliyekamatwa ni Dickson
Mshahili, muuguzi katika Hospitali ya Mkoa Kigoma ambaye katika upekuzi
nyumbani kwake, alikutwa na nyaraka mbalimbali ikiwemo madaftari 12 yakiwa na
kumbukumbu za vyeti anavyotengeneza na mihuri ya waganga wakuu wa mikoa ya
Kigoma, Kagera, Mwanza, Singida na Tabora.
Sambamba nao alikamatwa Zawadi
James, muuguzi wa Kituo cha Afya Ujiji ambaye baada ya kupekuliwa nyumbani
kwake, alikutwa na vyeti vitatu na kabuleta ya pikipiki ambayo hutumika
kutengeneza mihuri ya moto.
Wengine waliokamatwa ni Johnson
Nyabuzoka, mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Mlole ya mjini Kigoma, ambaye ni
mtaalam wa kompyuta aliyekuwa akitumika kufanya kazi hiyo; na Stephano Erasto
ambaye alikamatwa katika siku yake ya kwanza tangu ajiunge na duka hilo kwa
ajili ya kusaidia kazi. Mihuri iliyokamatwa katika tukio hilo.
Kompyuta mpakato,Laptop,Printer na
Scarner pamoja na mihuli ni vifaa vilivyokamatwa katika Steshanari hiyo